MAANA NA DHANA HALISI YA USHIRIKA


Nini maana ya ushirika......?

“Ushirika”, ni mkusanyiko wa watu walioamua kuungana kwa ridhaa yao wenyewe bila kulazimishwa kwa lengo la kusaidiana kupata mafanikio ya kiuchumi, kijamaa, kitamaduni na mahitaji mengine kupitia umiliki wa pamoja kwa kutumia demokrasia kwa wanachama wote.

Ushirika kama vyama vingine unaendeshwa katika misingi na kanuni zake katika kuhakikisha malengo husika ya ushirika yanatimia. Lakini pia thamani ya ushirika imejengwa kwenye misingi kadha wa kadha.

Thamani ya ushirika inajengwa juu ya kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, uwajibikaji wa kila mwanachama, upendo kwa kila mwanachama, demokrasia inayotoa haki sawa kwa wote, kuwa na umoja, usawa na mshikamano. Kwa kuzingatia hayo yote ndipo thamani ya ushirika inapopatikana.

Kanuni za vyama vya ushirika

Ushirika ukiwa kama taasisi ni lazima ziwepo kanuni zitakazotoa muongozo wa namna ushirika unatakiwa uwe ili kufanikisha malengo ya ushirika. Ushirika unaendeshwa kwa kuzingatia kanuni zifuatazo zikiwa kama sheria na muongozo;

Uanachama wa chama cha ushirika upo wazi na kwa kila mtu. Hii ni kanuni ya kwanza kabisa ambayo inatoa fursa kwa kila mtu mwenye akili timamu kuweza kuwa mwanachama wa chama cha ushirika chochote ili mradi aweze kukubaliana na mahitaji ya chama cha ushirika husika. Hii pia inatoa mwanaga kwa watu wa kada zote kwamba dhana ya ushirika inafanyakazi kwa kada zote, hapa namaanisha kunaweza kuwa na vyama vya ushirika vya wafanyakazi, vyama vya wakulima, ushirika wa wafanya biashara n.k

Demokrasia katika kusimamia na kuendeleza chama. Kuna dhana imejitokeza kwamba mtu mmoja anaweza kuanzisha chama cha ushirika na kuratibu kila kitu, hii si sawa hata kidogo! Chama cha ushirika sio taasisi ya mtu binafsi bali ni taasisi ya wanachama kimuundo na kiuendeshaji na kila mwanachama ana haki sawa katika chama! Hakuna aliyekuwa juu ya sheria au juu ya mwenzake. Hali hii inapelekea chama kuwa na amani, usawa, umoja na mshikamano muda wote.

Ushirikishwaji katika kujenga uchumi wa chama. Vyama vya ushirika vinamjenga mwanachama kuweza kujitegemea na kujua njia bora na sahihi za kutengeneza uchumi. Hali hii inatokana na darasa analopata mwanachama katika kujenga uchumi wa chama kwa kuchangia mtaji wa chama lakini pia ushiriki wake katika kusimamia na kuendesha mali za chama.

Uhuru. Chama cha ushirika kipo huru na wanachama wanasaidiana wenyewe kwa wenyewe bila kusubiri msaada wowote na bila masharti yoyote. Inapotokea chama kimelazimika kupata pesa au kuingia mkataba na taasisi yoyote nje ya chama basi zoezi kama hili linafanyika kwa kushirikisha wanachama wote kuwa na maamuzi ya pamoja.

Elimu, Mafunzo na kupeana taarifa baina ya wanachama. Kuwa kwenye chama cha ushirika kuna raha sana, wanachama wanapata fursa ya kupatiwa elimu na mafunzo mbalimbali ya kuwajenga kwa gharama ndogo sana. Wanapatiwa fursa za kuhabarishwa juu ya mambo mbalimbali yanayo endelea, taarifa za masoko, taarifa za uwekezaji n.k, hioi yote inafanyika ni katika kuwajengea wanachama uwezo

Ushirikiano na vyama au taasisi nyingine. Ushirika raha sana! Chama cha ushirika kinampa mwanachama fursa ya kushirikiana na vyama vingine au taasisi nyingine taasisi ambazo kwa mtu mmoja mmoja huenda ingekuwa ni vigumu kushirikiana nazo lakini kupitia ushirika mtu wa wa hali ya chini kabisa ambaye ni mwanachama wa chama cha ushirika anaweza akashirikiana na taasisi au mashirika mengine.

Kuzingatia maendeleo ya jamii. Vyama vya ushirika vinafanyakazi bega kwa bega kuhakikisha jamii inayoizunguka inapata maendeleo kutokana na uwepo wa chama cha ushirika katika maendeieo yao. Hii ni pamoja na kutoa ajira kwa wanajamii na kutoa huduma kwa jamii husika

Yote kwa yote hii inaonyesha ni kwa jinsi gani vyama vya ushirika vilivyokuwa kumuhimu kwenye jamii zetu

1 comment:

BENKI KUU YA USHIRIKA TANZANIA ''TANZANIA COOPERATIVE BANK......''

 Benki kuu ya Ushirika nchini Tanzania yenye makao yake makuu jijini Dodoma! inatazamiwa kuwa ni mkombozi wa vyama vya Ushirika nchini, Je, ...