VYAMA VYA USHIRIKA NI SULUHISHO LA UPATIKANAJI WA MASOKO KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI TANZANIA

Unaposikia neno “USHIRIKA” wengi wetu tunapata picha kwamba ni swala linalowahusu wakulima na ni kwa baadhi ya maeneo fulani tu! Dhana hii si kweli hata kidogo. Ushirika ni mfumo unaowaunganisha jamii fulani kwa hiari yao wenyewe bila kulazimishwa na mtu yeyote ili wawezekuunganisha nguvu zao kwa pamoja katika kutatua changamoto zinazo wakabili kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Vyama vya ushirika ni kiunganishi tosha kati ya serikali, wafanya biashara na wakulima vikitumika ipasavyo ni rahisi serikali kuwafikia wakulima moja kwa moja kusimamia miradi yake kwa wananchi lakini pia wakulima kuwafikia wasambazaji wa pembejeo na wateja. Moja ya kazi za vyama vya ushirika ni kutafuta masoko kwa wakulima na wafugaji, ni vigumu sana kwa mkulima ama mfugaji wa Tanzania mmoja mmojan kufikia soko la uhakika kulinganisha  na wakiwa kwenye chama cha ushirika. Mkulima peke yake ni ngumu sana kushindana sokoni kutokana na uhalisia wa dunia ya leo yenye teknolojia inayokua kila kukicha na udhaifu wa uchumi wake binafsi. Kuna vyama vya ushirika vya mazoa ya kahawa, pamba, mkonge tuliona jinsi vilivyo kuwa na nguvu kiuchumi, vyama kama Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU), Nyanza Cooperative Union (1984) Limited (NCU), Coastal Region Cooperative Union (CORECU), Morogoro Region Cooperative Union n.k, lakini pia tunaweza kuanzisha vyama vya ushirika kwa wakulima wa miwa kwenye viwanda vya sukari, wakulima wa mpunga, wakulima wa korosho, wakulima wa mbaazi, wakulima wa vitunguu, wakulima wa nyanya, wakulima wa maharage, dengu, wafugaji na wajasiriamali wetu.

Tanzania ipo kwenye ukanda wa jumuia ya Afrika Mashariki ambapo tuna soko la pamoja, wakulima, wafugaji na wajasiriamali wetu imekuwa ni vigumu kupenya kwenye soko kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya kuyafikia masoko husika, hii inatoa mwanya kwa wajanja wachache kunufaika na kuwaacha wakulima na wajasiriamali wadogo wakiwa hawana la kufanya. Hali hii inasababisha mambo mengi kutokea ikiwemo watu wa kati kuingilia kwa madai ya kuwasaidia wakulima wakati kiuhalisia wana wanyonya wakulima, taasisi mbalimbali kuingilia kwa lengo la kuwasaidia wakulima hali ya kuwa sio kweli!

Pongezi kwa taasisi ya SIDO inafanya jitihada kubwa sana katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watanzania wengi na ukweli ni kwamba elimu hiyo imewasaidia watanzania wengi wamekuwa wajasiriamali changamoto pekee ni namna ya kupata soko la ndani na nje ya nchi na hapa ndipo umuhimu wa kuwa na vyama vya ushirika unapokuja na kuwa mkombozi pekee wa kuwapatia masoko kwa kuwa na wataalamu wabobezi. Swala la wakulima na wajasiriamali kukosa masoko kwa bidhaa zao inaweza kupungua na/au kuisha kabisa kama serikali ikiweka kipaumbele na mipango mikakati madhubuti kupitia wizara ya ushirika na kilimo kutoa elimu ya vyama vya ushirika na kuvisimamia ipasavyo ili kuleta tija. Tuna vijana wengi wabobezi kutoka chuo pekee kinachotoa mafunzo ya vyama vya ushirika kwa ngazi za cheti, diploma na digrii ukanda wote wa Afrika Mashariki na kati, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ili kusaidia kuwa na vyama vya ushirika imara na vyenye nguvu kuwatetea wakulima, wafugaji, wajasiriamali na watu wa kada maalumu katika kufikia fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Kuna nchi  nyingi zilizo tuzunguka ambao wana uhitaji mkubwa wa vyakula kama mahindi. Baadhi ya nchi kama vile Sudani na Somalia wanauhitaji mkubwa wa mahindi lakini imekuwa changamoto kwa wakulima na wafugaji wetu kufikia hili soko. Nchi jirani kama Kenya wanatumia fursa hii ya kuchukua mazao utoka Tanzania na kufikisha kwenye hizi nchi hali ya kuwa wakulima wetu wanashindwa kupata maendeleo stahiki.

Nchi yetu ina utajiri wa mazao kama vile mahindi, vitunguu, nyanya, ndizi, maparachichi, mbaazi, miwa, pamba, korosho, dengu n.k ikiwekwa mipango thabiti wakulima na wafugaji wetu watapata kufurahia nguvu zao na kuongeza tija katika shughuli zao na hatimaye kuchangia pato la taifa kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment

BENKI KUU YA USHIRIKA TANZANIA ''TANZANIA COOPERATIVE BANK......''

 Benki kuu ya Ushirika nchini Tanzania yenye makao yake makuu jijini Dodoma! inatazamiwa kuwa ni mkombozi wa vyama vya Ushirika nchini, Je, ...